Kaimu mkurugenzi mkuu KEC aahidi kutatua changamoto Kibaha Sekondari

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Anathe Nnko ameahidi kushirikiana na uongozi wa Shule ya Sekondari Kibaha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia.
Hayo ameyasema tarehe 10/10/2024 akiwa mgeni rasmi kwenye Mahafali ya 57 ya Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibaha baada ya kusikiliza na kupokea risala ya wanafunzi wahitimu na taarifa ya shule hiyo.
“Shule imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne na cha sita. Ufaulu wa shule yetu kwa kidato cha nne ni asilimia 100 tangu mwaka 2015 hadi 2023. Na matarajio ya mwaka huu mwaka 2024 kwa wahitimu wa kidato cha nne ni shule kuwa katika kumi bora kitaifa,” amesema Bw. George Kazi ambae ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha wakati akitoa taarifa ya shule kwa mgeni rasmi.
“Changamoto kubwa zinazoikabili shule yetu ni upungufu wa vifaa vya maabara, uhaba wa vifaa vya michezo,” amesema Bw. Zaharuki Hamisi, mwanafunzi wa kidato cha nne, wakati akisoma risala ya wahitimu kwa mgeni rasmi.
Akijibu risala hiyo, Bw. Nnko ameahidi ofisi yake kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto hizo na kuwataka wazazi na wadau wengine kuunga mkono jitihada za walimu katika kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.
“Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa KEC pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha tutatua changamoto nilizozipokea na kwa kuanza amemuomba mkuu wa shule kufika ofisini kwake kuchukua mipira kwa ajili ya michezo. Aidha Nawasihi ndugu zangu, jukumu la kusimamia maendeleo katika elimu si la Serikali pekee, nawaomba wadau wote mkiwemo wazazi kutuunga mkono katika kufanikisha maendeleo mbalimbali ya shule yetu kwa kujitolea kwa hali na mali.” amesema Bw. Nnko.
Bw. Nnko pia amewapongeza wahitimu hao na kuwaasa kusoma kwa bidii ili kufanya vizuri katika mtihani wao wa Taifa. Aidha amewataka kuwa waadilifu kwenye jamii na kutumia ujuzi wao kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Nawapongeza kidato cha nne kwa kuhitimu masomo yenu, haya yote mtayafanikisha kama mtaendeleza nidhamu na kujituma. Kusoma kwenu kwa bidii kunawapa wigo mkubwa wa kuchagua taaluma yoyote kwa siku zenu za usoni na hatimaye tupate wataalamu na viongozi wakubwa katika taifa letu,”amesema Bw. Nnko.
Mahafali hayo yaliyohusisha wanafunzi wahitimu 104, yamefanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Kibaha inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha yakihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KEC Bw. Anathe Nnko, viongozi wa bodi ya shule hiyo, Menejimenti ya KEC, walimu, wazazi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha na Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.