Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

SHULE YA MSINGI TUMBI

Shule ya Msingi Tumbi

Shule ya Msingi Tumbi ni miongoni mwa shule nne ambayo inasimamiwa na Shirika la Elimu Kibaha ikiwa ni shule ya msingi pekee kati ya shule hizo. Shule hii ipo chini ya Kurugenzi ya Huduma za Elimu.

Shule ya Msingi Tumbi ilianzishwa mwaka 1966 ikiwa na wanafunzi 32 tu, na sasa shule ina kati ya wanafunzi 920 hadi 960. Shule hii ilianzia katika majengo ya Shule ya Sekondari Kibaha kabla ya kuhamia eneo hili ambako ipo sasa. Shule hii ilisajiliwa kwa namba PW/002 na namba ya usajili sasa ni EM.2689, ni ya kutwa na inachukua  wanafunzi wa kike na wa kiume. 

Mafanikio

Shule ya Msingi Tumbi ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya darasa la saba na darasa la nne. Kwa miaka zaidi ya 10 shule hii imekuwa ikipandisha wastani wa ufaulu kwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi. Vile vile, imekuwa ikifaulisha wanafunzi takribani wote na kwenda sekondari kila mwaka.

Huduma zinazotolewa

Shule ya Msingi Tumbi inatoa huduma ya ujifunzaji na ufundishaji na inatolewa kwa ubora wa hali ya juu.  Masomo yanayofundishwa ni; Kiingereza, Hisabati, Kiswahili, Sayansi na Teknolojia, Jiografia na Mazingira, Historia ya Tanzania na Maadili, Maarifa ya Jamii, Uraia na Maadili na Stadi za Kazi. Huduma inayotolewa darasa la kwanza ni; Kiingereza, Kusoma, Kuandika, Kutunza afya na Mazingira, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kuhesabu.

Shule inaandikisha wanafunzi kila mwaka na wanafunzi wa awali na darasa la kwanza wanaandikishwa wakitokea katika Kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto Tumbi. Wanafunzi huingia katika kituo hicho wakiwa na miaka mitatu hadi minne na kujiunga na darasa la awali wakiwa na umri wa miaka mitano na baadaye wanapokelewa darasa la kwanza wakiwa na umri wa miaka sita.