CHUO CHA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI KIBAHA
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha ni Chuo cha Serikali kikiwa ni moja ya taasisi za Shirika la Elimu Kibaha. Chuo hiki kilianzishwa mwaka 1968 wakati huo kikijulikana kama Chuo cha waganga wasaidizi vijijini. Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha kipo chini ya Kurugenzi ya Afya na kipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha. Kupitia mafunzo yanayotolewa na chuo kwa ngazi tajwa, dhana ya kutokomeza adui maradhi imekuwa ikitekelezwa kikamilifu kwa kuzalisha wataalam wa Afya ambao wanafanya kazi ndani na nje ya nchi katika sekta ya umma, mashirika na sekta binafsi. Chuo kinatoa huduma ya malezi kwa wanafunzi wa kiume na wa kike.
Usajili
Chuo kinasajili wanafunzi kati ya 80 hadi 100 kwa kila kozi kwa mwaka. Mwaka wa masomo unaanza Septemba kila mwaka.
Kozi za muda mrefu zinazotolewa:
- Stashahada ya utabibu
- Stashahada ya Uuguzi na Ukunga
Kozi za muda mfupi
- Wahudumu wa afya ngazi ya jamii
Mahali chuo kilipo
Chuo kinapatikana ndani ya Shirika la Elimu Kibaha karibu na Hospitali Rufaa ya Mkoa Pwani umbali wa takriban kilomita 1 kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.
Mafanikio
Chuo kimefanikiwa kutoa wataalamu wa afya ambao wanafanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Utaratibu wa kujiunga na chuo
Wanafunzi wanapata nafasi ya kujiunga kupitia njia kuu mbili ambazo ni:
- Kuomba kupitia dirisha la NACTVET ambalo zamani lilijulikana kama NACTE na linafunguliwa kila ifikapo mwezi Mei-June kila mwaka kupitia kiunganishi cha www.nacte.go.tz.
- Njia ya pili ni kupitia uchaguzi wa moja kwa moja kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne unaofanywa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Pia, chuo kinatoa nafasi ya kuhamia kwa wanafunzi wanaoendelea kutoka katika vyuo vingine nchini na nje ya nchi kupitia dirisha maalum ambalo hufunguliwa na NACTVET kila mwisho wa muhula kulingana na kalenda ya masomo kwa mwaka husika.
Kwa wanafunzi wanaojiunga na kozi ya muda mfupi ya Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (Community Health Workers), wanachaguliwa kwa utaratibu maalumu ambao unaratibiwa na ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Serikali za Mitaa katika mitaa na vijiji vyote Tanzania bara.
Sifa za kujiunga
Kwa kozi za Stashahada ya utabibu (Diploma in Clinical Medicine) na Stashahada ya Uuguzi na Ukunga (Diploma in Nursing and Midwifery), mwanafunzi wa kidato cha nne anatakiwa kuwa amepata ufaulu wa angalau alama C katika masomo ya Baolojia (Biology) na Kemia (Chemistry) na angalau alama D kwa somo la Fizikia (Physics). Pamoja na Masomo hayo mwanafunzi aliyepata alama ya PASS yaani angalau alama D kwa masomo ya Kiingereza (English) na Hesabu (Mathematics) atakuwa ameongeza nafasi ya ushindani kwa waombaji kwa mwaka husika.
Mwanafunzi, mzazi na wadau wanashauriwa kutembelea ukurasa wa NACTVET www.nacte.go.tz mara kwa mara ili kupata taarifa zinazohusu vigezo, muda wa kutuma maombi, taratibu za uhamisho pamoja na mambo mengine.
Mawasiliano:
Email: kibahacohas@kec.or.tz