Historia ya Shirika
HISTORIA YA SHIRIKA
Shirika la Elimu Kibaha ni Shirika la umma linalotoa huduma mbalimbali za kielimu. Lipo eneo la Wilaya ya Kibaha katika Mkoa wa Pwani yapata kilomita 40 Magharibi mwa Jiji la Dar es Salaam pembezoni mwa Barabara ya Morogoro.
Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa mwaka 1963 kama mradi wa pamoja chini ya wafadhili watano ambao ni Serikali ya Tanganyika kwa kipindi hicho, na nchi nne za Kinordic ambazo ni; Sweden, Denmark, Norway na Finland. Katika kipindi hicho mradi huu ulijulikana kama “Tanganyika Nordic Project” (TNP) mpaka mwaka 1970 ambapo mradi huu ulikabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha. Shirika lilianzishwa rasmi na kusajiliwa chini ya sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969, marejeo ya mwaka 2002.
Kwa mujibu wa Amri ya uanzishwaji wake, Shirika la Elimu Kibaha linaongozwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kwa mujibu wa kifungu 6 (1) cha Amri ya uanzishwaji wa Shirika, wajumbe wa bodi hiyo wanatoka katika Wizara zifuatazo;
- Wizara ya Kilimo
- Wizara ya Fedha na Mipango
- Wizara ya Afya
- Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
- Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu
- Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha na mjumbe mmoja kutoka Wilaya ya Kibaha anateuliwa na Bodi. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi anateuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha ndiye Mtendaji Mkuu na pia Katibu wa Bodi na huteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.