WENGI WATEMBELEA BANDA LA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA.

Wananchi wamejitokeza kwa wingi katika Banda la Shirika la Elimu Kibaha kupata taarifa mbalimbali za huduma zinazotolewa na Shirika.
Shirika la Elimu Kibaha ni moja ya Taasisi za Serikali zilizo chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambalo linashiriki kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma mwaka 2025.
Banda la Shirika la Elimu Kibaha, limetemebelewa na wananchi mbalimbali kutoka Jiji la Dodoma, Mkoa wa Morogoro, Kilimanjaro, Iringa, Pwani, Jiji la Dar es Salaam, na Mkoa wa Mara.
Kwa mujibu wa Mratibu wa maonesho ya Nanenane Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Sixbert Luziga, wananchi waliotembelea Banda la Shirika, wamepata taarifa ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi zinazounda Shirika hilo ambazo ni; Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Chuo cha Afya na Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Shule ya Sekondari Kibaha, Shule ya Sekondari Tumbi, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaha, Shule ya Msingi Tumbi, Kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto wadogo Tumbi na Maktaba ya Umma Kibaha.
Katika maonesho hayo, wananchi wamevutiwa zaidi na kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kinatoa kozi zifuatazo; ufundi umeme wa majumbani, ufundi bomba, ufundi magari, ufundi wa uundaji na uungaji vyuma (uchomeleaji), ufundi ujenzi, ufundi seremala, ufundi ushonaji wa mavazi na ubunifu wa mitindo, computer application, ujasiriamali, udereva, upishi na kilimo na ufugaji.
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha kinatoa kozi zifuatazo; Stashahada ya utabibu, Stashahada ya uuguzi na ukunga na Astashahada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii.