Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

DKT. MPANGO AZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2025 VIWANJA VYA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA.

Imewekwa: 03 Apr, 2025
DKT. MPANGO AZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2025 VIWANJA VYA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA.

Dkt. Mpango azindua mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amezindua mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.

Pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Alhaji Abubakar Kunenge, wananchi walijitokeza kwa wingi na kufanya sherehe za uzinduzi kufana.

Katika uzinduzi huo,  Dkt. Mpango amesema  mbali na uwepo wa kauli mbiu “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na Utulivu”, pia kuna mambo mengine matano ambayo  yatasisitizwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wakati ukikimbizwa katika Halmashauri 195 nchini.

Makamu wa Rais  amesema mambo matano ambayo yamepewa kipaumbele wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 ni pamoja na wananchi kuelimishwa kuhusu lishe bora kwa afya imara, mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya rushwa, na mapambano dhidi ya ukimwi. 

Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar zinaendelea kusimamia kwa dhati na kwa haki misingi ya demokrasia na kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba kushiriki uchaguzi kwa uhuru, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.