Wahitimu Watakiwa Kuwainua Vijana Kiuchumi

Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha- Kibaha FDC wametakiwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata chuoni ili kuwainua vijana wenzao ambao hawakupata ujuzi katika chuo hicho.
Kauli hii imetolewa tarehe 21/11/2024 na Mkurugenzi wa Elimu OR-TAMISEMI (ELIMU), Dkt. Emmanuel Shindika katika mahafali ya 52 ya chuo hicho ambayo yamefanyika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Dkt. Emmanuel Shindika amewataka wahitimu kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali kwa lengo la kupata fursa ya kuunganisha nguvu katika shughuli za uzalishaji mali.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassani imejipambanua vizuri katika kuimarisha uchumi, sera nzuri za kibenki, ukopeshaji na ushirika wa akiba na mikopo, hivyo tumieni fursa hizi vizuri, mkajiunge katika vikundi na kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri, lakini pia mwapatie vijana wenzenu ujuzi na pia endelezeni uchumi wa Taifa,” amesema Dkt. Shindika.
Akizungumzia ukarabati wa chuo, Dkt. Emmanuel Shindika amesema Serikali inaendelea kuboresha vyuo vya maendeleo ya wananchi kikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha na kwamba katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni mia nne (400,000,000/= kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho na tayari ukarabati umekamilika.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi ametoa pongezi kwa wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kwa kufanikiwa kumaliza mafunzo na amewashauri kutumia vizuri ujuzi walioupata kuboresha maisha yao.
Mkurugenzi wa shirika, Bw. Shilingi ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya wAamu ya Sita chini ya Raisi wetu Samia Suluhu Hassani kwa kuoa fedha taslimu shilingi millioni mia nne 400,000,000/= kwa ajili ya ukarabati wa miundo mbinu ya chuo hicho na tayari ukarabati umekamilika.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Bw. Joseph Nchimbi ameomba Serikali ikipatie chuo fedha za ruzuku kwa ajili ya chakula cha wanachuo na uendeshaji kama ilivyo kwa vyuo vingine vya FDC vilivyo chini ya Wizara ya Elimu.
“Tunaomba Serikali iendelee kutusaidia kutatua changamoto ya gari litakalorahisisha usafiri na usafirishaji hapa chuoni na kutupatia fedha za kufanya ukarabati na kuongeza majengo mapya yanayohitajika,” amesema Bw. Nchimbi.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Elimu Tamisemi Dkt. Emmanuel Shindika, Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw Robert Shilingi, Mkuu wa Chuo cha KFDC, wakurugenzi na wakuu wa idara na vitengo wa Shirika la Elimu Kibaha, wakufunzi na watumishi wasio wakufunzi wa KFDC, viongozi wa dini, wanafunzi na wazazi wa wahitimu wa chuo hicho.