Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

WAHITIMU WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA KUWA WAZALENDO

Imewekwa: 24 Apr, 2025
WAHITIMU WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA KUWA WAZALENDO

Wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Kibaha ambayo iko chini ya Shirika la Elimu Kibaha wameaswa kushikamana, kushirikiana na kuwa wazalendo, kwa kuwa umoja ni nguvu.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 24/4/2025 na Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Bw. Abdul Mombokaleo katika mahafali ya 58 ya shule hiyo ambayo yamefanyika kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha. 

Katika mahafali hayo, Bw. Abdul Mombokaleo amewasihi wahitimu kuipenda Tanzania kwa kuwa wajasiri na kuwa wapatanishi.

 "Kumbuka hamtakuwa wakamilifu bila kuwa waaminifu. Mbele yenu kuna dunia yenye nafasi na nafasi hiyo ni yenu, hivyo pambaneni kufikia ndoto zenu," amesema Mgeni rasmi, Bw. Mombokaleo.

Katika hatua nyingine, Mgeni rasmi  ametoa msaada wa kompyuta 25 ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Nae, Kaimu Mkurugenzi Mkuu  wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Anathe Nnko ametoa  shukrani kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Mombokaleo kwa kutoa msaada wa kompyuta 25 kwa Shule ya Sekondari Kibaha ambazo zitasaidia katika kujifunza na kufundishia.