Serikali kuendelea kuboresha maslahi ya walimu nchini.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuboresha maslahi ya walimu nchini kwa kuwa inatambua umuhimu wao wa utoaji wa elimu bora kwa Watanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi, Zainab Katimba (Elimu) wakati alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha ambalo linasimamia shule za Sekondari, msingi, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (Kibaha-FDC).
Katika ziara hiyo, Bi. Katimba amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kujenga nyumba za walimu na kupandisha madaraja kwa walimu mbalimbali.
“ Wote ni mashuhuda baada ya Mhe. Rais kuingia madarakani alianza kupandisha madaraja kwa walimu na bado anaendela. Upandishaji wa madaraja ni zaidi ya asilimia 200,” amesema Bi. Katimba.
Naibu Waziri, Bi. Katimba pia alipata nafasi ya kutembelea madarasa yatayotumika katika ufundishaji mbashara (live teaching) na kuona jinsi teknolojia hiyo inavyotumika.
“Teknolojia hii ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita ambayo itatumika ili kuhakikisha wanafunzi wengi waliojitokeza mashuleni hawakosi elimu,” amesema.
Bi. Katimba amewahakikishia walimu kwamba teknolojia hiyo haitawaondoa walimu kazini au kupunguza walimu kwani kila mwaka Serikali inaendelea kutoa vibali vya kuajiri walimu wapya.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi amemuhakikishia Naibu Waziri kwamba Shirika litaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia mapato ya ndani.
“Mhe. Naibu Waziri, Shirika la Elimu Kibaha tumefanikiwa kujenga madarasa mawili katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha kwa kutumia mapato ya ndani, lengo ni kuwawezesha wanachuo kusoma katika mazingira mazuri,” amesema Bw. Shilingi.